Chuo kikuu Ardhi chahimizwa kutumia wanataaluma wake kutatua changamoto za Ardhi nchini.

Chuo kikuu Ardhi chahimizwa kutumia wanataaluma wake kutatua changamoto za Ardhi nchini.

Chuo kikuu Ardhi kimetakiwa kutumia wanataaluma wake kuelekeza nguvu kubwa katika kukabiliana na changamoto na kutatua matatizo ya ardhi ambayo yanaathiri kwa kiasi kukubwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ya kufufua uchumi kupitia mpango wa “Tanzania ya Viwanda” unaolenga kuipelekea Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi wakati wa ufunguzi wa mradi wa kituo cha mtandao wa utawala bora katika sekta ya ardhi ukanda wa nchi za afrika mashariki (Network of Excellence in Land Governance in Africa, Eastern Africa) uliofanyika chuoni hapo ijumaa hii Oktoba 27, 2017.

Akizungumza kuhusu nafasi ya chuo hicho katika kuendeleza sekta ya Ardhi nchini, Lukuvi amesema chuo hicho ndio chuo pekee kinachozalisha wataalam katika sekta ya ardhi ambapo umefika wakati sasa wa kijitathmini ni kwa kiasi gani kimeweza kuchangia katika kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta ya ardhi.

“Sote tunatambua kuwa kuna changamoto nyingi za kiutendaji katika sekta ya ardhi. Ni mategemeo yangu kuwa kupitia mradi huu ambao ninauzindua leo wa kituo cha mtandao wa utawala bora katika sekta ya ardhi ukanda wa nchi za afrika mashariki (NELGA – Eastern Efrica Node), Chuo kama taasisi yenye wataalamu waliobobea kwenye fani za ardhi, kitatoa mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto hizi” alisema Mhe. Lukuvi.

Awali akitoa maelezo kuhusu mradi wa NELGA, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Prof. Evaristo Liwa alisema upatikanaji wa mradi huu katika Chuo Kikuu Ardhi ni matokeo ya ubobezi na uwezo wa chuo hiki katika masuala mbalimbali yanayoizunguka ardhi ambapo April 2016 kilichaguliwa na Umoja wa nchi za Afrika (AU) kupitia mradi wa “NELGA” (Network of Excellence in Land Governance in Africa, Eastern Africa) ili kuhudumia kama kitovu cha kuboresha mtandao wa elimu na mafunzo katika sekta ya ardhi “NELGA node” ukanda wa nchi Afrika Mashariki.

Fursa ambayo pia ilipelekea Chuo kupata ufadhili wa kuanzisha mradi wa kuboresha usimamizi katika sekta ya Ardhi kutoka Serikali ya Ujerumani. Ufadhili huu ulitokana na tafiti zilizofanywa na Umoja wa Nchi za Africa (African Union) kupitia kituo cha Mpango wa Sera ya Ardhi (The Land Policy Initiative – LPI) na kubainisha taasisi za kitaaluma bobezi katika masuala ya ardhi na mazingira ambapo pia ilibainishwa kuwepo kwa mapungufu katika utendaji kwa wataalamu wa sekta ya Ardhi katika Afrika.

Prof. Liwa alisema ili kufanikisha utekelezaji wa program hii Bara la Afrika limegawanywa katika kanda 5 mojawapo ikiwa ni Kanda ya Mashariki ya Afrika. Chuo Kikuu Ardhi kimechaguliwa kusimamia utekelezaji wa program hiyo katika ukanda huu ambapo Mradi huu unalenga kutekeleza Kukuza taaluma kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaochukua shahada za uzamili, Kuwezesha ubadilishanaji wa wanataaluma kwenye vyuo vishiriki kwenye mradi, Kutoa elimu na mafunzo kuziba mianya iliyoonekana katika tafiti zilizofanywa na Mpango wa Sera ya Ardhi (Land Policy Initiative), Kuchangia uboreshaji wa sera za ardhi katika nchi zinazoshiriki kwenye mradi na Kuanzisha mchakato wa ukusanyaji na utunzaji wa taarifa zinazohusu masuala ya ardhi katika Maktaba ya Chuo Kikuu Ardhi .

Mradi huu wa NEGLA ambapo ni sehemu ya ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la Maendeleo (GIZ) katika awamu hii ya kwanza ambayo imepangwa kutekelezwa katika kipindi cha miezi 18 kuanzia Agosti 2017 na imepanga kutumia jumla ya Euro 230,000. Pamoja na wageni wengine uzinduzi huu ulihudhuliwa pia na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) nchini Tanzania, Bw. Ernst Hustaedt

NO. 2Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa kabla ya uzinduzi wa mradi wa kituo cha mtandao wa utawala bora katika sekta ya ardhi ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

NO. 3Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiteta jambo na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) Bw. Ernst Hustaedt.

NO. 4Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa alipokuwa akitoa hotuba fupi ya kumkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi wa kituo cha mtandao wa utawala bora katika sekta ya ardhi ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

NO. 6Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Ardhi, wafanyakazi wa shirika la Maendeleo la Ujerumani na wageni waalikwa wakimsikiliza Makamu Mkuu wa Chuo pichani hayupo alipokuwa akitoa hotuba fupi ya kumkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi wa kituo cha mtandao wa utawala bora katika sekta ya ardhi ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

NO. 7Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) Bw. Ernst Hustaedt akielezea kwa ufupi GIZ na mradi wa mtandao wa utawala bora katika sekta ya ardhi ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

NO. 8Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi alipokuwa akisoma hotuba ya ufunguzi wa mradi wa kituo cha mtandao wa utawala bora katika sekta ya ardhi ukanda wa nchi za Afrika Mashariki (kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Evaristo Liwa na Kulia ni mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani GIZ Bw. Ernst Hustaedt)

NO. 5Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Ardhi, wafanyakazi wa shirika la Maendeleo la Ujerumani na wageni waalikwa wakimsikiliza mgeni rasmi pichani hayupo alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa mradi wa kituo cha mtandao wa utawala bora katika sekta ya ardhi ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

NO 10Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi mara baada ya kukata utepe kwa ajili ya uzinduzi wa mradi huo kulia ni mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani Bw. Ernst Hustaedt na mshauri wa shirika hilo Bw. Sostenes Katwale.

NO 11Picha ya pamoja ya washiriki wa mradi huo.

NO. 12Prof. Wilbard Kombe akiwasilisha mada ya chapisho la juu kwa ngazi ya uprofesa (Professorial Inaugural Lecture) isemayo “Tathmini ya mabadiliko ya kitaasisi katika nyanja ya usimamizi wa Ardhi katika nchi za Africa: Changamoto, Mapungufu na Fursa”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *