Chuo Kikuu Ardhi chaeleza ushiriki wake katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya uchumi na jamii nchini

Chuo Kikuu Ardhi chaeleza ushiriki wake katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya uchumi na jamii nchini

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa Mshoro ameelezea ushiriki wa chuo chake katika baadhi ya masuala muhimu ya nchi na kutokana na taaluma zinazofundishwa na kufanyiwa tafiti na chuo chake.

Ameeleza hayo jana alipokuwa na mkutano na waandishi na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa habari maelezo, alisema utafiti huu unahusisha ujenzi wa kuta za jingo kwa kumimina mchanganyiko mahsusi wa saruji, mchanga na kemikali maalum kwa kutumia kingo za plastiki (plastic formwork) zinazoweza kutumika hadi mara hamsini baada ya matumizi ya awali.

Aidha Prof. Mshoro aliendelea kufafanua kuwa ukuta wa aina hii hutumia mfupi katika ujenzi na hazihitaji plasta kabla ya kupaka rangi, unaruhusu kuezeka kwa muda mfupi na vipimo vya maabara vimeonesha kuwa unaweza kubeba uzito mara tatu zaidi ukilinganisha na kuta zingine zinazotumia tofali za kawaida.

Amesema mpaka sasa majengo yaliyokamilika kwa ujenzi huu wa gharama nafuu ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha ambayo ilizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa(Mb) tarehe 21 Septemba, 2016. Majengo mengine ya Mahakama yanaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali ya Kawe na Kigamboni.

Tafiti nyingine zilizofanywa na Chuo Kikuu Ardhi ni kupunguza athari za milipuko ya volcano ya  mlima Oldonyo Lengai ambao umehusisha kuweka vituo vitano (5) vyenye vifaa maalum kuuzunguka mlima ambavyo vimeunganishwa na mtandao wa intaneti ili watafiti waweze kupata taarifa sahihi ya hali ya msuguano wa miamba kwa wakati wote, tafiti ingine ni  ufuatiliaji wa tabia ya bahari katika bandari ya Tanga ili kusaidia kupatikana kwa taarifa sahihi kwa wakati wote ambazo baada ya kuzitathmini na kuzitolea taarifa zinazoweza kuwasaidia watumiaji wa bandari, wavuvi, watalii na watoa elimu kufanya maamuzi sahihi .

Prof. Mshoro alisema, Chuo Kikuu, Ardhi pia hutoa ushauri wa kitaalamu na huduma nyingine katika jamii kwa kutekeleza miradi mbalimbali kama ya usanifu na usimamizi wa ujenzi wa majengo marefu pacha ya PSPF Dar es Salaam, kufanya tathmini ya athari ya mazingira, uthamanishi mali na upimaji wa wa ardhi wa zaidi ya km 500 za upitishwaji wa bomba la gesi kutoka Mtwara, tathmini ya mji wa KIlosa baada ya kukumbwa na mafuriko, mlipuko wa mabomu ya Gongo la Mboto na Mbagala na kadhalika.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa Mshoro akizungumza na waandishi jana katika ukumbi wa habari maelezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *